Rotunda

Kuba la kuvutia, kuta za marumaru, sanamu kubwa, sakafu zilizonakshiwa kitajiri zikiwa na nyota ya Taifa Huru la Kongo – chumba hiki cha duara kinafanana na hekalu la Leopold wa pili na miradi yake ya kikoloni. Kati ya mwaka 1910 na 1966, mashubaka yalijazwa na kazi za Wachonga sanamu wa Kibelgiji.

Kazi zilizo maarufu zaidi ni zile nne za kati zilizosanifiwa na Arsène Matton (1873 - 1953). Sanamu hizo zinawakilisha maono ya kikoloni. Wabelgiji wanaelezewa kama vile ni wafadhili na watu walioistaarabisha Kongo kana kwamba hawakutenda baya lolote juu ya nchi hiyo na kana kwamba kulikuwa hakuna ustaarabu wowote kabla hawajawasili. Waafrika wanawasilishwa wakiwa wadogo kulinganishwa na Wazungu au shughuli walizozifanya zinawasilishwa kwa uchache. Wanawake wa Kiafrika wanawasilishwa kama vyombo vya ngono. Mfanyabiashara wa Kiafrika mwenye asili ya Kiarabu anaoneshwa akimkanyaga Mkongomani ambaye anajaribu kumlinda mkewe. Hii ni moja ya propaganda zilizoshikiliwa za kikoloni ambazo hata sasa zinaendelea kuwa na athari hata baada ya karne nzima kupita.

Sanamu katika mashubaka hayo ni sehemu ya urithi unaolindwa na hauwezi kuhamishwa. Makumbusho yalimwalika msanii wa Kikongo Aimé Mpane kutengeneza mradi utakaotumika kukinzanisha sanaa hizo na sanaa mpya inayoonesha mtazamo tofauti. Msanii huyo alibuni sanamu mbili zinazotazamana, moja ikidokeza kuhusu heshima ya zamani (Fuvu la Lusinga) na nyingine ikitoa ahadi ya wakati ujao mwema (Pumzi mpya au Kongo inayoongezeka). Mpane baadaye, alifanya kazi sanjari na Msanii wa Kibelgiji Jean Pierre Muller kutengeneza RE/STORE, seti ya pazia kumi na sita za kuangaza zilizofunikwa kwenye sanamu zilizopo ili kuleta maana mpya.

< World Kiswahili Day